JE, NI LAZIMA KUWA MJUMBE WA KANISA ILI USAIDIWE?
Na John Msafiri – Mwanafunzi wa Maisha, Mchambuzi wa Imani na Mwanachama wa Jumuiya ya “Waliotengwa kwa Ukimya”
Kuna siku nilienda kushiriki mazishi ya rafiki yangu kule kijijini. Msiba ulikuwa mzito, huzuni iliweza kung’oa nywele, lakini kilichonigonga zaidi ni pale rafiki yangu mmoja – tuseme jina lake ni Oti – aliposimama kutoa rambirambi akasema:
“Huyu ndugu alitengwa na jumuiya kwa sababu hakushiriki. Lakini leo tuko hapa kumzika. Je, ni lazima afe ndiyo atambulike kuwa ni wetu?”
Watu wakacheka kwa aibu. Wengine wakatikisa vichwa. Lakini ukweli ulikuwa pale pale: kwanini tunawapa watu kinywaji cha baraka baada ya safari yao, badala ya wakati bado walikuwa na kiu?
1. Kanisa ni Hospitali ya Wenye Kiu, Siyo Klabu ya Wenye Machozi ya Mbele
Katika dunia ya leo ya hashtag gospel na WhatsApp fellowships, tunaweza kuamini kuwa imani ni jambo la mtu binafsi. Lakini kama Biblia inavyotuambia:
“Tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine.” – Waebrania 10:25
Kweli ni kwamba, ushiriki katika jumuiya au mashirika ya Kanisa hujenga muungano wa kiroho, unaofanana na sockets zinazoshikilia mwanga wa taa. Bila hiyo socket, hata taa ya dhahabu haitaangaza.
Lakini swali letu la leo ni: Je, kama mtu hana hiyo socket ya jumuiya, hapaswi kupewa stima ya msaada?
2. Msaada wa Kanisa ni Kama Mchele wa Arusi – Hauchagui Nani Amekaribishwa
Katika arusi nyingi za Kiafrika, ukifika wakati wa chakula, hakuna mtu anaulizwa “umetoa mchango kweli?”
Wanaulizwa: “Uko na sahani?” 😄
Ndivyo msaada wa Kanisa unavyopaswa kuwa. Mtu akiwa na haja – ya mwili au ya roho – sahani yake ya kiu na uchungu inapaswa kuwa tiketi yake ya kusaidiwa.
Kumbuka hadithi ya Yesu kuhusu Msamaria Mwema?
Yule mtu aliyepigwa na majambazi hakuulizwa, “Ulikuwa unashiriki synagogi?” Alisaidiwa – na si kuhani, bali ni mtu wa mbali.
Yesu hakusema, “Wasaidie walioko kwenye list ya CWA.”
Alisema, “Nilikuwa na njaa, mkanipa chakula.” – Mathayo 25:35
3. Kushiriki ni Muhimu, Lakini Usihukumu Waliobaki Nje ya Kuta
Tuseme ukweli. Kuna ndugu zetu wamekaa kimya si maadamu ni wavivu, bali wamekosewa kanisani. Wengine walichelewa mara tatu mfululizo wakaitwa “baridi,” wengine walionekana hawatoi mchango wakakosa kuchaguliwa hata kusalimiana.
Kuna wale walikataliwa eti hawana suti ya Kwaya, au waseja “kwa Kanisa.”
Lakini usimfananishe mtu anayeogopa kurudi kanisani na yule anayeikimbia imani. Hali si tabia.
Kama Petro alimkana Yesu mara tatu na bado akapewa nafasi ya kulisha kondoo, basi hata hawa “wanaokaa nyuma ya Kanisa” wanapaswa kupata msaada wa kiroho na mwili.
4. Kanisa La Leo, Linapaswa Kuwa Kama Mama – Halichagui Mtoto wa Kukumbatia
Kanisa likianza kugeuka kuwa sehemu ya burudani yaani Klabu ya walio sahihi, tutapoteza maana ya Injili.
Yesu aliwasaidia wazinzi, watoza ushuru, wagonjwa na waliokataliwa – bila kuuliza “ulitoa sadaka wiki iliyopita?”
Kama Yesu angekuwa Katibu wa Jumuiya Ndogo Ndogo, hangekusanya watu waliopendelewa. Angeanza na waliojeruhiwa.
Kwa hiyo Kanisa letu, liwe bandari ya huruma, si booth ya kupima ushiriki wa Jumapili.
5. SULUHISHO: Tuwapokee Walio Nje, Tuwaimarishe Walioko Ndani
Ni kweli — watu wanapaswa kushiriki jumuiya, kwa sababu:
-
Hapo ndipo wanajifunza Neno.
-
Hapo ndipo wanajulika shida zao.
-
Hapo ndipo huduma hupangwa.
Lakini pia ni kweli:
-
Msaada wa Kanisa usiwe na masharti ya kiwanachama.
-
Upendo usiwe wa wale wanaovaa sare pekee.
-
Neema isigawiwe kwa walio “seen” kwenye attendance book.
Kama mtu aliyeanguka hajulikani kwa sababu hakushiriki, ni wajibu wetu kumtafuta.
Kama Kanisa takatifu haliwezi kusaidia mtu kwa sababu “hatutamjua,” basi tusisahau kuwa hata Yesu alimsaidia yule mama Msamaria wa kisimani ambaye hakuwa wa jumuiya yoyote.
“Mti haujui nani atakula kivuli chake — lakini bado huota.”Hivyo ndivyo Kanisa linapaswa kuwa.
Tusibague. Tusihukumu. Tukumbatie.
Kwa sababu siku moja – wewe au mimi – tunaweza kuwa upande wa pili wa msaada.
Na tutajua, Kanisa halikuwa genge la wachache, bali mwili wa Kristo wenye mikono iliyofunguka kwa wote.
Wewe je?
Je, umewahi kuona mtu akikataliwa kwa sababu ya kutoshiriki?
Ama wewe mwenyewe ulishawahi kujisikia kama “mgeni kwenye nyumba ya Baba”?
Tuandikie, tushirikiane.
Kanisa ni letu sote.
™©•® Johπ PoetKeyα Msαfiri 2025
JOHN MSAFIRI
Spoken Word Poet | Media Relations Concierge | Strategic PR & Communications Specialist | Seasoned Writer | Thespian | Playwright | Copyrighter | Domestic Scandal Evangelist
Comments
Post a Comment